Malumbano ya Uke
Duncan Mwangi
Duncan Mwangi
Aliahidi kuwa atajiunga naye.
Forsyth amesimama kando ya kituo cha garimoshi kama wenzake wenye hamu ya kuingia mji wa Tokyo, iwe kwa kazi ama kwa ziara. Ni mji ambao anautambua kama umbo wa vidole vyake. Anajua pa kupumzisha kichwa na pa kukanyagisha guu. Anajua ni wapi pana supu ya pweza iliyokolea na wapi pana mikate inayokatika na urahisi wa ndizi lililoiva. Anajua ni maghorofa yapi yaliyowachwa wazi bila mtu ndani na kujaa matundu yanayoelekeza miale ya jua ndani kama miale ya laser, miale ambayo amewahi kuona kwenye sinema za kijambazi tu.
Leo amechelewa akichelea. Zimepita garimoshi angalau tatu, moja kwa kila nusu saa. Anamsubiri Mwende, msichana ambaye hamjui ndani nje, bali tu ni mweusi kama yeye. Tokyo hawapo wengi. Walisahibiana katika sherehe za kazini. Mwende ni mwuzaji wa bima za watalii. Anafanya kazi kwa kampuni kubwa hapa mjini. Forsyth kaalikwa sherehe na aliyemuuzia bima yake, Louie, aliyemwahidi sharti wasichana weusi wangekuwa. "Vile ninavyokualika ndivyo wataalikana."
Hata hivyo sherehe ile haikufana walivyotarajia. Mpango wa idara ya wafanyikazi ulikuwa kuwakalisha kiti na kuwakabidhi bilauri nyembamba za champagne wakiyaskiza yaliyotukia mwakani. Ikawabidi waondoke mmoja mmoja kwa utaratibu wapatane nje ya ofisi kisha waende wajitafutie raha yao, raha iliyowaelekeza kwenye ghorofa lake Mwende walipobugia vileo aina ya tequila kwa vijikombe vidogo vya kauri na kuchezea muziki wa hiphop. Wakiwemo wanamuziki mashuhuri mpindua santuri alicheza, Forsyth aliweza kuwatambua Fat Joe na Ll Cool J kwa sababu anawaenzi. Forsyth akasonga kando yake Mwende na akacheza karata yake kisha wakatongozana chumbani na kujisalimisha kwa ukware uliokuwa umewapanda.
Sasa amevaa nguo zinazositiri umbo lake. Anayo kabuti nyeusi na suruali yenye upana mkubwa nafasi zake nusura zimtoshee ndovu. Hata ingawa sio mara yake ya kwanza katika zahanati ya kuavya mimba, pana tofauti kadhaa. Yeye bado ni mgeni, hata na mazoea yake ya mji huu. Ujasiri aliokuwa nao siku zake za chuo kikuu kule Atlanta umempotea. Haina maana kuwa anajuta kwani hakuna la kujuta. Nafasi angepewa ya kurudi bado hatima ingekuwa ile ile. Hata hivyo anaogopa. Anaogopa watu. Anaogopa sheria ambayo ingawa inasusia utendakazi, bado kwa maandishi yake inakataza.
Garimoshi linafika. Watu wanapanga foleni kuingia. Forsyth anaitoa simu yake mfukoni mwa suruali yake kubwa na anampigia Mwende. "Umekaribia wapi?" Mwende anamjibu kuwa bado yupo nyumbani. Udhaifu wa sauti yake unamjulisha Forsyth kuwa simu yake ndio imemrausha.
Baada ya majadiliano yao, ambapo Mwende anamwahidi kuwa atapiga simu kwa dereva wa teksi badala ya kujisalimisha kwa mfumo wa usafiri wa umma, Forsyth analiabiri garimoshi na kuketi kando ya mwanamume kijana mwenye kimo sawa na yeye. Mwanamume huyo mwenye asili ya Kijapani anasoma gazeti. Masikio ameyavalisha vipuli vikubwa vya chuma vinavyoning'inia kwenye ndewe kama migomba ya ndizi. Amevaa shati yenye mikono mifupi inayoonyesha chale zilizochanjwa kwenye mkono wake wa kulia. Forsyth anasoma maneno hayo yaliyoandikwa mkononi kwa wino. Jeremiah 29:11. Ni shairi lililo katika ncha ya ulimi wake, na linalomkumbusha ujana wake alipokuwa mwanasabato. Shati amefungua vitufe viwili kuonyesha kifua chake chenye usawa unaokinzana na matiti yake, matiti yanayodhihirisha kuwa anapenda kupiga mazoezi.
Abiria aliyekuwa ameketi mkabala wao anashuka punde garimoshi linaposimama katika kituo cha kwanza. Mara moja, mwanamume aliye kando yake Forsyth anasimama na kubadilisha kiti, gazeti mkononi, huku akimtupia Forsyth jicho la kumchukia. Jicho hili linamfahamisha Forsyth kwamba hajafurahi kukaguliwa.
Forsyth anaamua kuyaelekeza mawazo yake kwake Mwende na jinsi alivyokubali kuhusiana naye kama mvukajinsia, haswa kimapenzi. Ana mjomba Mzambia ambaye, ingawa anamkubali, alimwambia watamaduni kule Afrika wangeuchukia uume wake. Mjomba huyo wake, Elisaphan, anasoma shahada ya uzamili katika masomo ya kijinsia kule chuo kikuu cha umma cha Massachusetts Amherst. Kila mara anampa ilani kuwa ajihadhari anapohusiana na Waafrika. Elisaphat ana mume anayeitwa Harold, mume aliyeoa kwa siri na ambaye bado hajamfichua kwa wazazi wake kila anaporudi nyumbani Zambia. Kwa muda mrefu, Forsyth alimdhania kuwa mpangaji kwani gharama ya kodi walikoishi Boston ilikuwa kubwa sana.
"Ni busara kuhofia maisha yako. Hata mimi ingawa nilitamani kumpeleka Harold kwa wazazi bila kuwapa maelezo makubwa kuhusu uhusiano wetu, nilifahamu kuwa muda ungefika ambao tungesahau na tukumbatiane ama tubadilishane mate na kujikwaza."
Kwa muda ambao wamehusiana, Forsyth hana hoja na Mwende. Awe mtamaduni, awe msabato kama Forsyth katika ujana wake, hata awe na bwana wa siri, yote haidhuru. Amefurahi kutamaniwa. Hakuna azimio kubwa zaidi kwake. Anataka hawa wasichana wa watu kumpepesea kope na kummezea mate kama kipande cha halua. Hatamani harusi wala joto kitandani kila usiku; hayo ni matamanio ya kichatu.
Garimoshi linasimama Ikebukuro. Amefika. Mwanamume yule mvalia-vipuli na mchanjwa-chale ananyanyua miguu yake kutoka mvunguni mwa kiti kama ishara ya kusimama. Forsyth inambidi asubiri kisha afuate. Hapo ndio mwanzo wao kufuatana, nyayo kwa nyayo hadi zahanati ya kuavya mimba ya Yamateotsuka.
Tukio hili la kibahati linamshangaza.
Forsyth anatafuta kiti kwenye sebule ya kupokea wageni. Pana kochi mbili zinazounda herufi ya L na maua ya alizeti ambayo yamepandwa ndani ya chungu kirembo cha samawati. Wasichana wawili wenye asili ya Kijapani wameketi pale wakiwa wanakumbatiana. Pia kuna wazee: babu ambaye anasinzia na bibi anayechezea kiganja cha kulia cha babu yule. Katikati ya sebule ni meza ndogo iliyojaa majarida ya Kijapani. Mwanamume yule wa garimoshi yupo kwa karani wa mapokezi akimnong'onezea.
Alikitoa kijusi chake katika msimu wa joto katika zahanati iliyokuwa na viyoyozi ili kupunga hewa. Anakumbuka jinsi ambavyo jua ilivyomwangazia kwa ukali alipokuwa akielekea nyumbani, nusura imkemee kwa chaguo lake. Alichemka. Ilimbidi dereva wa teksi kuingia dukakuu na kumletea maji, na hayakumfaa hata. Alipofika chumbani mwake katika chuo kikuu, hali ya kichefuchefu ilimzidia. Mwanafunzi aliyekuwa amepanga naye alimpata amepiga magoti kando ya choo anatetemeka. "Uduvi kakuharibikia tumbo?" alimwuliza.
Bahati ya Mwende kumpata mtu wa kuwa naye zahanatini ilimfurahisha pamoja na kumsikitisha Forsyth. Alisikitikia kukumbuka ile hali yake ya zamani.
Mwanamume yule wa garimoshi anapinduka kujitambulisha (anaitwa Hansuke) kisha anaashiria kila anayetaka kutoa uzazi amfuate. Forsyth anainua mkono kuuliza, "Na je ikiwa ninamsubiri?"
"Usiwe na wasiwasi. Subiri tu papo hapo. Atakapowasili mtajiunga nasi," Hansuke anamjibu.
Mapokezini pana runinga inayoashiria ubadilishaji wa fedha za kigeni katika kituo kinachoitwa Sun TV. Yeni inabadalishana na dola kwa gharama ya yeni mia moja na sita kwa dola moja. Anakumbuka Mwende akimwambia kuwa Kenya na Japani zinakaribiana kwa ubadilishaji huu lakini uchumi zao ni ardhi na bingu. Forsyth, ambaye ni mhitimu wa masomo ya uchumi, naye katamka, "Pesa ni kama jinsia. Zote ni udanganyifu mkubwa tu."
Ingawa Mwende mara nyingi alisusia kuyafumbua maisha yake kwa Forsyth, siku hiyo alimwambia kuhusu wazazi alioacha.
"Mama yangu wa kambo ndiye aliyenipa jina Mwende. Kusudi ya mama yangu mzazi ilikuwa kumwoa mama wa kambo na kushirikiana na baba yangu kunizaa kwa binafsi yake. Majirani wetu wadini wanaiheshimu ndoa ile, hata kama inakinzana na maadili yao."
Forsyth akayatafakari aliyoambiwa. Maswali mengi yalimzonga. "Mama yako mzazi je ana neno?"
"Hata."
"Sharti baba yako anaona haya kuwa bibiye pia ana bibi."
"Bibiye pia ana mikono na halioni jambo."
Mwende kisha akayatupa macho yake kifuani mwa Forsyth, kifua chenyewe sambamba na kimeota vinywele. "Jinsia udanganyifu mkubwa sio?"
Forsyth akafuata macho yake Mwende hadi yalipofika kwenye uchi wake. Nyusi zake akazitikisa juu chini kuitikia kauli.
"Mbona basi haja ya kuvuka?"
***
Mwende anawasili baada ya saa moja na nusu akiwa amevalia dera ya rangi nyeupe iliyonakshiwa kwa maua ya bluu, iliyo na upindo unaofagia chini anapotembea. Mkononi ana pakiti mbili za kaukau za ndizi. Anamkabidhi Forsyth pakiti moja na kujitandaza kando yake. "Niwie radhi kwa kuchelewa."
"Haina neno. Nimekuahidia siku yote, na hata ingalikuwa mbili ningalikupa. Mimi ni mtalii tu hapa. Sina miadi wala majukumu ya kazi."
Wanampata Hansuke ofisini mwake akicheza wimbo mmoja wa Fat Joe ambao Forsyth anauenzi na ambao unawashirikisha Ashanti na Ja Rule. Wimbo wenyewe unauiga wimbo mashuhuri wa mwaka wa 1984 uliotungwa na mwanamuziki Tina Turner, lakini umebadilishwa mfumo na mizani ili uwavutie wasikilizaji wa kisasa. Hansuke anawaona wamesimama mlangoni anapomaliza kupanga faili juu ya kabati lililo nyuma ya dawati lake. Anaizima sauti ya wimbo inayotoka kwa simu yake mahiri iliyowekwa dawatini.
"Karibuni sana. Ninatumai mko salama," anawasalimu huku anamtupia Forsyth jicho lile alilompa walipokuwa kwenye garimoshi. Labda anajihoji kimoyomoyo, anauliza ikiwa yeye ni shoga kutokana na alivyomkagua ama ni mpenda wanawake kutokana na jinsi yeye na Mwende walivyounganisha mikono. Labda anamfahamu kutoka siku zake za awali na anachukizwa na uanaume wake. Labda pia yeye ni mvukajinsia anayetaka kumtambua mvukajinsia mwenzio kama anavyojaribu Forsyth, na sharti himaya zinamvaa. Mwende, ambaye hayajui yanayojiri kati ya wanaume hawa wawili, anajibu salamu za Hanzuke kwa shauku zake.
Katika mchakato wa mazungumzo yao, Forsyth anakumbuka sauti ya kipazasauti ikitua alipokuwa akipewa ushauri nasaha kabla ya kusahihisha cheti kilichothibiti kauli yake. "Haja kwako kukifuta kitoto, haja ya Mungu lazima itatimia!" Kisha dirisha la jumba walimokuwa likavunjika kwa kishindo na vigae kutapakaa. Tofali lenyewe liliangukia sinia la vifaa vya upasuaji vilivyonadhifiwa.
"Ni ubaridi tu," Forsyth anawaambia waja hawa wawili wanaoangazia macho jinsi anavyotetemeka.

Duncan Mwangi ni mhitimu wa masomo ya uandishi ya Nairobi Fiction yanayoongozwa na mshindi
wa tuzo la Caine, Makena Onjerika.
wa tuzo la Caine, Makena Onjerika.