Karakana ya Kheri
Wesley Tsuma
Wesley Tsuma
“Hivi itanigharimu pesa ngapi ikiwa nitataka majeneza saba sasa hivi?" Haya ndiyo maneno aliyosema Hamisi baada tu ya kutufikia kazini petu. Paji lake la uso nalo likiwa limekunjamana kuashiria uzito wa maneno yake, na pengine dharura aliyokuwa nayo.
Kabla kujibiwa kwake kimya cha mda kilitanda mle ndani asitake mtu kuzungumza. Ilikuwa ni kitambo sana tangu mteja atujie akiagiza kununua majeneza mawili. Huyu wa leo si mawili, si matatu wala hata manne, anaagiza saba tena kwa mpigo. Pameondokea ajali wapi wakaaga watu saba na hivyo akayahitaji? Alafu tena hata tukimuuzia, atayasafirishia nini kwani petu amekuja mikono mitupu, tena akitembea. Ndiyo baadhi tu ya maswali yasiyopata majibu niliyokuwa nayo akilini.
Mda si mrefu baadaye Babu alifanya hima kumhudumia mteja. "Salama sana mkuu, kwa majeneza saba utahitajika kutoa takribani shilingi laki tatu kulingana na yale utakayochagua, uko radhi kutoa fedha hizo au vipi?" Alimjibu babu baada ya kuteuwa maneno yake kisawasawa asije kumuudhi mteja wetu. Wakati huu swali lililozidi kujirudia rudia akilini mwangu ni wapi haswa pamefiwa watu saba pakahitajika majeneza kwa dharura. Hamisi alikuwa anayapeleka wapi? Ukweli usemwe ijapokuwa ili kufaidika kwetu kwa kuuza majeneza palihitajika kufa watu, hata kwa siku moja tusingempigia dua Maulana akaipokonya dunia wanadamu wengi hivi.
"Haya sawa acha niyakague kabla kuyanunua," alisema Hamisi huku akielekea nje ya karakana tulikokuwa tumeyapanga majeneza hayo kisawasawa kuwavutia wateja. "Jiskie nyumbani mkuu," akamjibia babu huku akitabasamu.
Wakati wote huu Hamisi akiyakagua majeneza ungelimwangalia Babu ungeliona bayana shauku aliyonayo. Naye pia kama mimi tu alionekana kustaajabishwa na vijimambo vya Hamisi. Lakini ilitubidi kuficha mshangao wetu asije akatuona Hamisi akajihisi kuwa ng'ombe palipo na wanadamu. Aliyakagua majeneza hayo na baada ya kuridhishwa na alichokiona akataka kuyalipia. Alikuwa anakamilisha biashara hii ya majeneza Babu alipomuuliza Hamisi swali lile lile nililoshindwa kulitamka.
"Hivi bwana majeneza haya unayapeleka wapi haswa?" aliuliza Babu akielekeza mkono wake wa kushoto alipokuwa amesimama Hamisi. Swali hili aliloelekezewa Hamisi lilimchenga akilini kwani alichukua mda kabla kumjibu. Ghafla akaanza kutokwa na machozi jambo ambalo lilimpelekea Babu kumketisha chini ili kumliwaza na pengine kufahamu analia kwa nini.
Mda si mrefu baadae Hamisi akaanza kulonga.
"Mimi bwana mwanzo naitwa Hamisi na natokea mtaa wa Uyoga. Kabla kuja kwako hapa nilikuwa nimetembelea karakana kadha wa kadha mtaani kwetu nikiazimia kununua majeneza yaya haya ila hakuna seremala aliyetaka kunishughulikia. Sikujua ni kwa nini walifanya hivyo ila walizidisha misononeko niliyonayo moyoni. Maisha yangu ya utotoni hayakuwa ya mabegi makubwa makubwa ya kheri bali mapipa ya matatizo chungu nzima. Nilizaliwa katika familia ya watoto wanne, wa kiume wawili sawa na wa kike wawili. Nilikuwa na matarajio makuu ya mapenzi tele kutoka kwa wazazi na familia yangu kwa jumla. Hata hivyo, kwao nilikuwa laana waliolimbikiziwa kwa kosa wasilolijua. Kwa hiyo, penzi la mama ama vile la wazazi sijawahi kuushuhudia. Badala ya kunyonya titi la mama nilipewa chai ya mkandaa, moto, na iliyokosa sukari. Badala ya kulazwa kitandani nililazwa katika zizi la ng'ombe, juu ya malisho yao ya nyasi zilizokauka na kwa hiyo zilinidunga dunga kila nilipozilalia. Manukato ya kuzuia ngozi yangu kuchibuka kutokana na miale ya jua sikupata japo yanapeanwa bure kupitia serikali. Nilipojisaidia kwenye nguo zangu nilipewa kichapo na mwili wangu ukaishia kuwa na vidonda vilivyochukua mda kupona. Niliwekwa mateka zizini huku ndugu zangu wakienda shule kupata elimu iliyokuwa ya bure. Ndugu zangu walipoenda kucheza na wenzao niliamriwa nioshe vyombo vya pale nyumbani na baadae niwe dobi. Nilipewa mrundiko wa nguo ijapo nilikuwa na umri wa miaka saba. Mateso haya kutoka kwa wazazi wangu yalinizalishia dharau kutoka kwa ndugu zangu. Hata yule kitinda-mimba alitaka nimwite mheshimiwa. Takribani mwezi mmoja uliopita alitutembelea chifu wa kata letu akiandamana na mwanasiasa niliyeskia wakimwita Jomba. Baada ya mazungumzo ya mda nilihisi ngurumo fulani, kama vile kwato za watu zikielekea zizini nilikokuwa. Mlango ulipofunguliwa nlimwona babangu, chifu na bwana Jomba aliyeniashiria kwa mkongojo wake kwa dharau...”
Wakati huo akizungumza babu aligundua mdomo wake Hamisi uliyokaukiwa mate. Akaniagiza nimletee maji mgeni wetu. Kitambo kidogo baadae baada ya kumletea maji, akapiga funda kadhaa, aliendelea kutufumbulia kisa chake akiwa ni mwenye nguvu zaidi.
“Asanti sana kwa maji, kiu kilikuwa kimenikaba koo kwelikweli. Kwa siku kadhaa zilizofuata chifu pamoja na bwana Jomba wakawa wageni wa kawaida pale nyumbani. Kila siku wakija na kuzungumziana faraghani na wazazi wangu. Wakati mmoja nililetewa mahamri matatu na bwana Jomba. Nikayala kwa pupa kwani nilikuwa nahisi njaa ajabu. Baadae nilianza kuhisi kichwa kikiniwanga, tumbo nayo ikinisokota. Bwana Jomba alikuwa amenipa sumu. Nilizirai na nilipopata fahamu nilijikuta maskani pa mchawi, nikiwa uchi wa mnyama, mikono na miguu yangu ikiwa imefungwa nisisonge hata kidogo, juu ya madhabahu, chini yangu naye mchawi mwenyewe akitayarisha moto tayari kwa kazi, kunitoa mimi kama sadaka kwa mizimwi ili wazazi wangu watajirike. Nilianza kujuta kuzaliwa kwangu humu duniani. Mbona mamangu asingeiavya mimba yangu? Mbona Mungu aniachie niendelee kuteseka. Baada ya kufanya ishara ya msalaba nilikuwa tayari kwenda akhera. Ghafla nikaanza kuhisi kamba ikilegezwa. 'Waliokuleta hapa wameondoka kabla hawajalipa ada ya mizimwi niliyowaagiza ili kufanikisha kazi yao. Kwa hiyo, mizimwi imekasirika sana. Toka hapa mara moja kabla nibadili mawazo yangu.' Hii ilikuwa sauti ya uhuru na sikusita kuifuata mara moja. Nilijikwamua na kutoka mbio nisijue naelekea wapi japo akilini na moyoni nilitaka sana kulipiza kisasi kwa wazazi na jamii yangu. Njiani maseremala wengi hawakunihudumia. Sijui walidhani sina pesa za kulipia bidhaa nilizoulizia au vipi? Hivyo ndivyo nlivyokutana nawe baada ya kutembea kwingi nikisaka wa kunihudumia.”
Mda wote huu Hamisi akizungumza nilijikuta nalia kwa hiari, mashavu yangu yakishamiri vijistari vya machozi. Nikimwangalia Babu huzuni ilijichora wazi usoni pake. Pengine asingeweza kutokwa na machozi kwa sababu ya ukavu wa ngozi yake ya kizee. Kama huu ndio uhalisia wa mambo basi kuishi kwingi sio kuona mengi pekee bali pia ni kulia kwingi.
"Hivi bwana nimekuskia kwa makini sana. Amakweli moyo wangu umepevuka. Niulize swali moja tu, ningekuwa babako mzazi ungetaka nikutendee nini?" aliuliza babu. Tabasamu nalo likamvaa uso Hamisi akijitayarisha kumjibu babu yangu.
"Mkuu kwa kweli nikushukuru sana kwa kunipa sikio kwa makini. Ikiwa ungekuwa babangu ningependa sana mwanzo unisaidie kuzika maisha yangu ya kale katika kaburi la sahau. Nitafurahia sana kama nitapata nafasi ya kwenda shule, kuwa na familia inayoniheshimu na kunipenda bila kunitenga au kunibagua kwa misingi wa kuwa zeruzeru. Nikipata haya mkuu nitashkuru."
"Safi sana, hata hivyo ningependa ujue kwamba duniani hapakosekani matatizo ya hapa na pale. Hata hapa petu tunakumbwa na masaibu kadha wa kadha ila inatubidi kukaa ngumu. Pole sana kwa yale uliyoyapitia mikononi mwa wazazi na jamii yako. Ama kwa kweli cha mtu huliwa na mtu, chuma tu ndo huliwa na kutu. Hata hivyo, utapendaje kuwa mmoja wetu, kuishi nasi, kufanya kazi hii papa hapa na sisi?"
Kwa mara nyingine nilimwona Hamisi akitabasamu. Mara hii tabasamu lenyewe likiwa bora hata zaidi. "Nitafurahia sana mkuu, Maulana akubariki sana kwa moyo wako huu mkunjufu waliopewa wachache sana na Mungu wakati wa kuiumba dunia. Nashkuru sana.”
Hivi sasa ni wiki moja tangu Hamisi aungane nasi. Kupitia kwake karakana yetu imepata umaarufu hata zaidi. Utawasikia watu wakisemezana “tunaenda pale kwa Hamisi.”
Wesley Tsuma is a young Kenyan, currently a third year student of Journalism and Mass Communication at Masinde Muliro University of Science and Technology. He is passionate about a changed society in terms of a society without rape cases, inequality instances, corruption, poverty and other vices. Through his articles and poems he hopes to reach many people and thereafter achieve his objective: a changed society.